Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Kuzaliwa kwa Bibi Zaynab (s.a), binti tukufu wa Amirul-Mu’minin Ali bin Abi Talib (a.s) na Bibi Fatimah Zahra (s.a), ilikuwa ni tarehe 15 Jumada al-Ula mwaka wa tano wa Hijra katika mji mtukufu wa Madina.
Kuzaliwa kwake katika familia yenye watu wakubwa mno katika historia ya Uislamu kulikuwa ni mwanzo wa kuzaliwa kwa mtu ambaye hatima yake ilikuwa ni kuleta mustakabali wenye nuru na uliojaa mafunzo na mawaidha makubwa kwa Waislamu. Jina la “Zaynab” lililochaguliwa kwake, lenye maana ya “mapambo ya baba”, lilikuwa ni ishara ya hadhi yake ya juu mbele ya baba yake mtukufu.
Hadhi na Sifa Binafsi
Bibi Zaynab (a.s) alilelewa katika malezi ya baba yake Ali bin Abi Talib (a.s), shujaa na kiongozi wa waumini, na mama yake Fatimah Zahra (s.a), binti wa mmoja wa watu wakubwa kabisa katika historia ya Uislamu. Mazingira hayo yalimpa fursa ya kunufaika na elimu ya dini na vielelezo bora zaidi vya utu. Kwa kiwango hicho cha elimu na hekima, alijulikana kwa lakabu ya “‘Alimah ghayru mu‘allamah” – yaani mwanamke mwenye elimu ya kina na pana bila kuwa na mwalimu wa kufundishwa rasmi. Hakuwa na upeo wa juu tu katika elimu ya dini, bali hata katika falsafa na maadili alikuwa katika nafasi tukufu.
Nafasi Kuu ya Uongozi
Tukio la Karbala lililotokea tarehe 10 Muharram mwaka 61 Hijria lilikuwa uwanja wa kudhihirika kwa nafasi ya kihistoria ya Bibi Zaynab (a.s) kama kiongozi shujaa na imara. Baada ya tukio hilo lenye uchungu, alijitokeza kama msimamizi hodari na kiongozi mahiri. Katika mazingira magumu, alisimama kwa ujasiri na uthabiti dhidi ya dhulma za Yazid na wafuasi wake, na akawasilisha ujumbe wa wazi wa Karbala kwa vizazi vya baadaye.
Kwa hotuba zake zenye nguvu katika kasri la Yazid, aliweza kukifikisha kilio cha uonevu aliofanyiwa ndugu yake Imam Husein (a.s) na familia yake katika jamii yote. Maneno yake ya moto, yenye hekima na ujasiri mkubwa, yaliangaza katika giza la ukandamizaji, yakawa sauti ya ukweli isiyozimika licha ya manyanyaso na mateso yote.
Mafundisho Yake
Bibi Zaynab (a.s) hakuonekana tu kama mwanamke wa kidini, bali kama alama ya kujitolea na kusimama dhidi ya dhulma. Mafunzo na sifa zake kama vile ujasiri, kujitolea, upendo kwa familia, na utetezi wa haki na ukweli, vimemfanya kuwa kielelezo cha milele kwa nyakati zote.
Hotuba zake katika kasri la Yazid, zilizojawa na hoja zenye mantiki na hisia za kibinadamu, zilidhihirisha ukweli wa tabia yake na zikabeba roho ya mapinduzi ya Karbala hadi katika nyoyo za watu. Kwa kujitolea kwao wanafamilia wake, aliuonesha ulimwengu maana halisi ya “Ithar” (kujitoa kwa ajili ya wengine).
Athari za Kitamaduni na Kijamii
Kuzaliwa kwa Bibi Zaynab (s.a) halikuwa tukio la kifamilia tu katika nyumba ya Ahlul-Bayt (a.s), bali lilikuwa na athari kubwa na ya kina katika historia ya Uislamu. Kama kielelezo cha kiutamaduni na kijamii, aligeuka kuwa mfano bora kwa wanawake Waislamu katika historia.
Bibi Zaynab (a.s) aliwafundisha wanawake kwamba wanaweza kusimama kwa heshima na ujasiri mbele ya changamoto, na akaunda mtazamo huu ndani ya jamii. Mtazamo huu haukuishia kwa wanawake Waislamu tu, bali hata kwa wafuasi wa dini nyingine, akawa chachu ya uundaji wa jamii yenye kujitolea kwa maadili na utu.
Kujifunza maisha na mwenendo wake kunaweza kuwa mfano bora kwa vizazi vyote katika kukabiliana na matatizo na misukosuko ya maisha.
Athari kwa Mustakabali
Bibi Zaynab (a.s) hakuwa tu mwenye ushawishi katika zama zake, bali kutokana na ujumbe wake, aliweka alama ya kudumu katika historia na utamaduni wa Kiislamu. Alikuwa chanzo cha msukumo kwa wahusika wa kihistoria na vizazi vya baadaye, akiwafundisha kutokukubali dhulma na kusimama kwa ujasiri katika njia ya haki na ukweli.
Mafunzo yake ya kijamii, kama yalivyokuwa muhimu katika zama zake, leo bado ni chemchemi ya kuleta motisha kwenye harakati za haki na mapambano dhidi ya dhulma na ukosefu wa usawa katika jamii mbalimbali.
Sherehe na Maadhimisho
Katika ulimwengu wa Kiislamu, kuzaliwa kwa Bibi Zaynab (a.s) kunahesabiwa kama tukio adhimu na huadhimishwa kwa kufanyika sherehe maalum kwa ajili ya kumkumbuka mwanamke huyu mashuhuri. Maadhimisho hayo si tu yanakumbusha hadhi yake tukufu, bali yanatoa fursa ya kutafakari na kujifunza kutokana na mafunzo yake.
Wakati wa sherehe hizi, waimbaji wa kaswida na washairi hutaja fadhila zake, kuhadithia miujiza na kujitolea kwake, na hivyo kuyakuza mafunzo ya Kiislamu na utu kwa kuiga tabia yake tukufu.
Kwa Muhtasari
Kuzaliwa kwa Bibi Zaynab (s.a) si historia tu, bali ni hatua muhimu katika mageuzi ya kibinadamu na kijamii. Kwa kuikumbuka siku hii, tunaweza kuimarisha ari ya kiroho na kisaikolojia katika jamii na kubadili mitazamo ya watu.
Yeye aliinua hadhi ya mwanamke katika Uislamu na akageuza tabu na matatizo kuwa fursa za ukuaji na maendeleo. Kwa kutegemea mafunzo ya mwanamke huyu mtukufu, tunaweza – kama taifa lenye umoja na lenye kushikamana na maadili – kupiga hatua kuelekea ujenzi wa jamii yenye haki na ubinadamu wa kweli.
Maoni yako